Sepp Blatter alazwa hospitali baada ya kupata mshituko
Rais wa shirikisho la Soka la kimataifa, Sepp Blatter aliyesimamishwa kwa siku 90 kujishughulisha na masuala ya soka kwa kashfa za rushwa, amelazwa hospitali kutokana na kupatwa mshtuko wa neva.
Blatter amelazwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya lakini sasa imeelezwa ataendelea kubaki huko. Awali ilidaiwa alikuwa na matatizo ya msongo wa mawazo hivyo ikabidi apate huduma ya matabibu, sasa imebainika ana tatizo la mshtuko wa neva.
Awali, mwanasheria wake, Richard Cullen alieleza juu ya uangalizi huo wa madaktari kutarajiwa, lakini akasema alitarajia arejee nyumbani mapema kabla hali kubadilika na kutolewa maelezo tofauti.
Hata hivyo, watu wake wa karibu wameeleza hali yake si mbaya na anatarajiwa kurejea katika hali ya kawaida japokuwa atabaki hospitalini hadi mapema wiki ijayo.
Msaidizi wake, Walter Gagg, amesema kwamba bosi huyo anatarajiwa kuwa mwenyeji wa hafla ya kukabidhi tuzo ya mwanasoka bora hapo Januari 11 mwakani.
Post a Comment