Image result for tigo banner

Magufuli atishia kuwatumbua jipu mawaziri wawili walioanza na JK


Operesheni ya kutumbua majipu ya Rais John Magufuli nusura iwaangukie Mawaziri wawili ambao walikuwa mawaziri pia katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Taarifa kutoka katika chanzo cha kuaminiwa zimeeleza kuwa Rais Magufuli alionesha kutoridhishwa na utendaji wa Mawaziri hao na kuwafokea mbele ya mawaziri wenzake kwa kuwataja majina katika kikao maalum cha mawaziri kilichofanyika hivi karibuni.

“Wewe (anataja jina la Waziri) na mwenzako (anamtaja jina pia) nitawatumbua,” Chanzo cha gazeti la Rais Mwema kinamkariri Rais Magufuli.

Chanzo hicho kilieleza kuwa Rais Magufuli aliwaonya pia mawaziri wengine ambao alionesha kutoridhishwa na utendaji wao kwakuwa hawaendani na kasi yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“Magufuli anataka atoe mfano kwa mawaziri wengine kwamba wao si watu maalum sana. Kama wanavyotumbuliwa watu wengine na wao pia wanaweza kutumbuliwa,” kiliongeza chanzo cha gazeti hilo.

Rais Magufuli aliunda Baraza lake la Mawaziri mwishoni mwa mwaka jana na kuwashauri wasifanye sherehe ya kuteuliwa kwakuwa wakifanya vibaya hatawaonea haya atawaondoa mara moja bila kujali majina yao.

Utendaji wa Rais Magufuli umeendelea kusifiwa kila kona hususan katika kuwawajibisha viongozi wa ngazi zote na kuonesha nia ya dhati ya kuwahudumia watanzania huku akipambana na uzembe na ufisadi.

No comments

Powered by Blogger.