Image result for tigo banner

Wanao Uza Wasichana Nje ya Nchi kwa Kisingizio cha Kuwatafutia Ajira

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiR2ZFytiZJH5c59-ZG_U5dzgbmc1Sf0EIrZqSGUr1IQDJQztEPB3WMRZfYNg-dgIY9y6BG_Py98WX-U1nGEoW_zW-pF2brCDiSSSzRXEgKIEMuctkYDL6PF7-kjGJONuwbXUo2oIA4G9Cx/


 SERIKALI imepata majina ya baadhi ya wahusika wa mtandao wa kimataifa unaohusika kusafirisha na kuuza nje ya nchi wasichana wa Kitanzania wa miaka kati ya 16 na 24, kwa kisingizio cha kuwatafutia ajira.

Aidha, imesema tayari mawasiliano na serikali za nchi wanakopelekwa wasichana hao yamefanyika kuhakikisha wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu wanachokifanya ni biashara haramu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga alieleza Bunge jana akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Balozi Mahiga aliweka wazi kuwa katika orodha wamo Watanzania wanaoishi nchini na wengine nje ya Tanzania wanaoshirikiana na wageni. Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, kufanikiwa kupata majina hayo kumetokana na ushirikiano kutoka kwa Jumuiya za Watanzania waishio nchini Thailand na India pamoja na waathirika wa biashara hiyo haramu.

“Kwa hapa nyumbani uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na balozi za nchi ambazo wasichana wetu wanapelekwa ili kubaini watu wote walio sehemu ya mtandao huo, hususan wanaowezesha upatikanaji wa vibali vya kusafiria kwenye balozi hizo ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria,” alisema Balozi Mahiga.

Alisema tayari serikali imeziomba balozi hizo ziwe makini zaidi kudhibiti uombaji wa vibali vya kusafiria kwa shughuli mbalimbali na kuwataka wahusika kuthibitisha uwezo wa kifedha walionao kufanya utalii, kufanya shughuli au kuishi kwenye nchi wanazokwenda ili kuudhibiti mtandao huo.

Alisema, wanamtandao hao wanaojihusisha zaidi kuuza watu ili washiriki ukahaba, huwanyang’anya, kushikilia pasipoti za wasichana wanaowarubuni na kuwadai Dola za Marekani 5,000 hadi 6,000, baada ya kuwafikisha wanakowapeleka, jambo linalokuwa gumu kutekelezwa na wasichana hao kwa kukosa fedha, hivyo kujikuta wakikubali kufanya biashara ya ukahaba.

“Ninatoa mwito kwa Watanzania wote tuwe makini pale tunapopata fursa za kazi nje ya nchi. Ni muhimu kuzingatia na kujiridhisha kuhusu masuala ya msingi yanayohusu ajira za nje ikiwa ni pamoja na kuwepo mkataba rasmi wa ajira unaotambuliwa na mamlaka husika zilizopo nchini na za nchi ambayo mtu anataka kwenda,” alisema.

Alitoa rai pia kwa Watanzania wanaokwenda nje kufanya kazi kujisajili kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania uliopo katika nchi hizo na kutokubali kuweka hati za kusafiria rehani. Balozi Mahiga aliwataka wananchi waelewe kuwa ahadi nyingi za ajira kwa nchi za Thailand, Malaysia na China zinatolewa na watu wasio waaminifu wanaoshiriki katika mtandao wa biashara haramu ya watu.

Aidha, alisema bado kuna Watanzania kadhaa wanatumikia vifungo na adhabu ya kifo katika magereza ya nchi mbalimbali duniani baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Alitaja nchi waliko na idadi yao kwenye mabano kuwa ni Brazil (41), China (266), Iran (68), Thailand (14) na Umoja wa Falme za Kiarabu (3).

No comments

Powered by Blogger.