Diamond: Haikua rahisi kujifunza kiingereza lakini ilinibidi
Miaka kadhaa iliyopita, Diamond Platnumz alijikuta kwenye mtihani mgumu baada ya kubaini kuwa hakutakiwa tu kutumbuiza kwenye jukwaa la kimataifa, bali pia alitakiwa kuzungumza kwa dakika kadhaa mbele ya live television Afrika nzima!
Kuongea hakikuwa kitu kigumu kwa muimbaji huyo wa Nana, bali lugha aliyotakiwa kutumia – Kiingereza, ilikuwa inampita kushoto wakati huo.
“Wakati naanza shughuli za muziki, nasema sasa nataka kwenda international, lilikuwa ni suala gumu sana,” Diamond alisema wakati akihutubia kwenye mahafali ya darasa la saba ya shule ya Righway ya Dar es Salaam alikoalikwa kama mgeni mashuhuri Jumapili, Oct 18.
“Nakumbuka mara ya kwanza nimeenda Big Brother kuperform, Tale ananiambia ukishamaliza kuperform utaulizwa maswali. Mimi nikamwambia meneja wangu Babutale, yale maswali yataulizwa live pale, nitazungumza nini? Ilikuwa mtihani. Cha kujibu ilibidi niambiwe nikikariri kwanza ili nikiweke kwenye kichwa, ilikuwa kazi kubwa sana,” alisimulia Diamond.
“Nikajiuliza nikasema, mimi nataka kwenda international muziki wetu wa Tanzania, Bongo Flava ufike mbali, sasa ntaufikisha vipi ikiwa lugha [Kiingereza] mgogoro? Palikuwa na kazi hapo! Kila nikijaribu kubabaisha naona hapana, akili inaniambia Diamond unatakiwa utafute mwalimu.”
“Nikasema I need to go back to school, nikajifunze. Wakati natoa hilo wazo kwa baadhi ya watu na wasanii wenzangu wakawa wananicheka wanasema elimu ya ukubwani, walikuwa wananicheka sana. Nikasema kila mtu na mipango yake, niachane na mipango yangu, nikawa namuita mwalimu ananifundisha pale japokuwa ratiba yangu ilikuwa inabana nasafiri sana lakini napopata muda najifunza,” aliongeza.
“Namshuru mwenyezi Mungu, sio kikubwa lakini kidogo nilichokifikia kinanisaidia sana. Wasanii sasa wanaanza kuniambia yule mwalimu wako anaitwa nani, niunganishe na mwalimu wako nawaambia ‘it’s too late you know.’
Post a Comment