Msafiri : Muongozaji wa video kutoka Tanzania anayetazamwa zaidi 2016 kufanya maajabu.
Katika fani ambayo mambo hugeuka haraka sana na tena kila mwaka,
nadhani uongozaji wa video unaongoza. Hii ni fani ambayo aliyekuwa namba
moja mwaka jana, mwaka unaofuata hawezi kubweteka tena, infact taji
lake huchukuliwa bila yeye mwenyewe kutarajia.
Wameshawahi kuja waongozaji wengi wa video nchini, wapo waliopotea
kabisa na kuamua kubadilisha fani na wapo wanaoendelea kufanya kazi
nzuri. Ningependa kwanza kusema kuwa hadi sasa ni muongozaji mmoja tu wa
video ambaye anapewa ile title ya ‘hall of fame’ kwa mchango mkubwa
alioufanya kwenye video za Tanzania. Naye si mwingine bali ni Adam Juma.
Adam ni P-Funk au Master J kwenye video za Bongo kwahiyo heshima yake
itabaki pale pale.
Lakini walikuja kuibuka waongozaji wengine miaka mitatu iliyopita
ambao wamekuja kubadilisha kabisa upepo wa video za muziki. Mwaka 2014
ulikuwa mwaka wa Nisher hadi kupelekea kushinda tuzo ya muongozaji wa
video anayependwa mwaka huu. Nisher alikuwa na hasira na mawazo mapya
katika ufanyaji video. Video kama Nje ya Boksi, Jikubali, Nakomaa na
Jiji na zingine zilionesha uwezo wa muongozaji huyu wa Arusha.
Nisher pia aliweza kuinspire vijana wengi waliopenda aina yake ya
uchukuaji na umaliziaji wa video. Lakini kiti chake kilikuja kuchukuliwa
mwaka 2015 na hasimu wake, Hanscana. Mwaka huo pia Hanscana alichukua
tuzo ya muongozaji wa video anayependwa kwenye Tuzo za Watu. Video kama
Nasema Nawe, Siri na zingine kibao, zilimpandisha chati na kumfanya kuwa
muongozaji anayetafutwa sana. Mwaka huu pia Hanscana ameongoza video
kali ikiwemo Fundi ya Mheshimiwa Temba na Kama Utanipenda ya Darassa na
zingine.
Lakini mambo yamebadilika tena, na hakika mwaka huu ni wa muongozaji
mwingine. Mwaka huu ni wa Msafiri aka Travellah wa kampuni ya Kwetu
Studios. Msafiri si mgeni kwenye video za muziki wa Tanzania. Naamini
amekuwepo hata kabla ya Nisher na Hanscana lakini hakufanikiwa kuwa mtu
anayezungumzwa sana kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya
kijamii kama wenzake.
Ameongoza video kibao za Hemed PHD na Jerry wa Rhymes na hapo mwanzo
ilionekana kuwa wawili hawa ndio waliokuwa wanauelewa zaidi uwezo wake.
Lakini mwaka huu, Msafiri – jiwe walilolikataa waashi, limegeuka mkate.
Amekuja tofauti sana na kwa muda mfupi tayari amekuwa muongozaji wa
video anayetafutwa zaidi.
Si kitu kilichotokea ghafla tu, lakini video zake mpya zina utofauti mkubwa.
Mwaka huu Msafiri amewashtua watu kwa video kibao kali zikiwemo Jike
Shupa ya Nuh Mziwanda, Chafu Pozi ya Billnass, Pesa ya Madafu ya Jay
Moe, Mboga Saba ya Mr Blue f/ Alikiba na zingine.
credit: Bongo5
Post a Comment