Kamati ya Maadili ya TFF yamfungia Mkurugenzi wa habari wa Yanga 'Jerry Muro' kujihusisha na soka.
MKUU
wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro
(pichani) amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja
na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3, baada ya kikao cha Kamati ya Maadili
ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kilichokaa leo kwenye Makao Makuu
ya Shirikisho hilo, chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde
Muro amefungiwa baada ya kukutwa na
hatia katika mashitaka mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa na TFF
mbele ya Kamati ya hiyo, ambayo ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu
ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya
kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo, akahukumiwa kutengana
na kutojihusisha na masuala ya soka kwa mwaka mmoja, wakati shitaka
lingine ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa
Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
Katika shitaka hilo, Jerry alidaiwa
kuwashawishi mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu
yao na kutowapa nafasi watani wao wa jadi (Simba) kuingia kwenye mchezo
huo ambao timu yake ilifungwa bao 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka huu
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jerry Muro alifanikiwa
kuishinda TFF katika shitaka la kupingana na maamuzi ya shirikisho hilo
juu ya masuala ya utoaji wa haki za matangazo ya Televisheni.
“Kamati ilisikiliza kwa makini taarifa
zake alipokuwa anazungumza na vituo vya Redio na kugundua alikuwa
sahihi, hivyo hapa hana hatia,”kimesema chanzo.Hata hivyo, Jerry Muro
amehukumiwa wakati mwenyewe hakuwepo kwenye kikao na inadaiwa hakutoa
taarifa ya maandishi juu ya kutohudhuria kwake.
Badala yake, imeelezwa Katibu wa
Yanga, Baraka Deusdedit alifika mapema leo kabla ya kikao kwa ajili ya
kutoa taarifa ya mdomo kwamba Muro amekwenda kwao Kilimanjaro kusafisha
makaburi ya wazee wake.
Lakini Kamati ikaamua kuendelea na
kikao kwa mujibu wa kanuni na hatimaye kuchukua hatua ilizochukua. Hata
hivyo, Muro ana haki ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya TFF.
Post a Comment