Miili ya wanajeshi wa Uganda yawasili
Miili ya wanajeshi 10 wa Uganda, waliouawa na wapiganaji wa al-Shabaab, nchini Somalia imesafirishwa nyumbani.
Msemaji
wa jeshi, Kanali Paddy Ankunda, amesema shambulio hilo "limebadili
mambo" na al-Shabaab wanafaa kutarajia "jibu lifaalo".
Wanajeshi
12 wa Uganda waliuawa kwenye shambulio hilo la Jumanne, kwenye kambi ya
wanajeshi wa Muungano wa Afrika (AU) Kusini mwa Somalia.
Al-Shabaab walisema waliua wanajeshi 70 wa AU.
Wanajeshi wa Uganda wamo kwenye kikosi cha wanajeshi 22,000 cha AU, kinachokabiliana na wapiganaji hao nchini Somalia.
Kwenye tamko la kwanza kabisa kutoka kwa jeshi la Uganda kuhusu
shambulio hilo, Kanali Ankunda alisema kupitia mtandao wa kijamii wa
Twitter: "Hatutalegeza juhudi zetu za kusaidia kurejesha amani Somalia
licha ya shambulio hilo." Hakutoa maelezo kuhusu miili ya wanajeshi hao
wengine wawili waliouawa.
Ripoti nyingine zinakadiria wanajeshi
waliouawa kwenye uvamizi huo katika kambi ya Janale, kilomita 90 Kusini
Magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, ni kati ya 20 na 50.
Wakazi
wanasema shambulio hilo lilianza kwa shambulio la kujitoa mhanga
lililotekelezwa kwa kulipua gari lililotegwa bomu kwenye lango la kambi
hiyo, na kisha kukawa na ufyatulianaji wa risasi uliodumu zaidi ya saa
moja.
Licha ya kupoteza ngome nyingi kusini na kati mwa Somalia, al-Shabaab
wameendelea kushambulia vikosi vya serikali na Muungano wa Afrika pande
mbalimbali nchini humo.
Wapiganaji hao pia hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara ya kujitoa mhanga Mogadishu.
Post a Comment