LOWASSA aitikisa ARUSHA leo.
Mgombea
Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha
Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Edward Lowassa ameendelea na kampeni
kanda ya kaskazini ambapo leo amefanya mkutano mkubwa jijini Arusha
kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Sinoni.
Lowassa
anayeungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wasomi pamoja na vijana
amewaambia wakazi wa mkoa wa Arusha kuwa ameamua kugombea Urais kwa kuwa
anachukia umaskini.
Lowassa amesema kazi yake ya kupambana na umaskini ataianza kwa kutoa elimu bure mpaka chuo Kikuu.
“Nitaanza
na elimu ili kuondoa hali ya umaskini. Vipaumbele vyangu vya kwanza
elimu pili elimu tatu elimu. Ukimpa mtoto wako elimu umemsaidia
kimaisha. Nimesema elimu kuanzia nursery hadi chuo kikuu bure,” amesema
Lowassa.
“Wanasema
haiwezekani mimi nasema inawezekana kabisa tuna fedha nyingi sana nchi
hii kuanzia gesi mpaka madini na utalii. Hakuna mwanafunzi kulipa
mchango wa aina yoyote. Nitazingatia maslahi ya mwalimu ili awe na moyo
na kazi yake.”
Lowassa
pia ameahidi kuboresha maisha ya wakulima kwa kupanua masoko ambapo
atawaruhusu wakulima wauze mazao yao mahali yanapopatikana masoko bila
vikwazo.
Wamachinga, bodaboda na mama ntilie nao hawakuachwa, ameahidi kuwawekea mazingira rafiki ya kufanya biashara zao.
“Mama
ntilie na machinga watakuwa rafiki wa serikali yangu. Naahidi nikiingia
ikulu baada ya wiki moja tu nitakuwa nimelidhughulikia tatizo lao la
maeneo ya biashara. Nitaanzisha benki kwa ajili ya kupata mikopo ya riba
nafuu.”
Lowassa
pia ameahidi kujenga Hospitali za rufaa kila wilaya ambazo zitakuwa na
vifaa vyote muhimu pamoja na dawa ili kuwaondolea wananchi adha ya
ukosefu wa huduma muhimu za matibabu hasa vijijini.
Aidha,
katika mkutano huo, mwanasiasa mkongwe wa chama cha Mapinduzi(CCM)
Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alijitoa ndani ya chama hicho wiki
iliyopita alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi.
Kingunge
amesema CCM imepoteza dira, haiwajali tena wananchi amesema hata kwenye
kampeni zao wanatumia muda mwingi kuzungumzia watu badala ya kuzungumza
masuala.
Amesema yeye ni mmoja wa watu wanopenda kuona mabadiliko katika Uchaguzi wa mwaka huu.
Kingunge
amebainisha kuwa jitihada kubwa zilifanywa na vyama vya TANU na ASP
kuboresha maisha ya wananchi hadi kuungana na kuunda CCM.
Amesema
juhudi hizo zimeendelea kufanywa katika awamu zote za uongozi lakini
amesema uongozi wa awamu ya nne umesaliti jitihada hizo.
Akitolea
mfano ukuaji wa uchumi; Kingunge amesema wakati rais wa awamu ya tatu
Benjamini Mkapa anaondoka madarakani uchumi ulikuwa unakua kwa asilimia
7%, Mkapa alichukua madaraka kutoka kwa Rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi
uchumi ukiwa unakua kwa asilimia 4%.
Amesema
kwa mujibu wa takwimu za Serikali za hivi karibuni uchumi wa Taifa
unaongezeka kwa kasi ya karibu asilimia 7, na kusema kuwa Taifa
halijasonga mbele katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Amesema CCM imechoka, imeishiwa pumzi ya kupambana na matatizo ya wananchi hivyo ni wakati muafaka kwa chama hicho kupumzishwa.
Kingunge
amewataka wananchi kutofanya makosa tarehe 25 Oktoba kwa kufanya uamuzi
sahihi wa kumchagua Edward Lowassa kuwa Rais wa Tanzania pamoja na
wagombea wa nafasi mbalimbali kutoka vyama vinavyounda UKAWA.
Viongozi
wengine waliohutubia katika mkutano huo ni Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Waziri Mkuu
mstaafu awamu ya tatu, Fredrick Sumaye.
Akihutubia
katika mkuano huo, Sumaye amesema kuwa chama cha Mapinduzi kimeharibu
elimu pia kimeshindwa kuwapatia vijana ajira baada ya kuuwa viwanda.
Amebainisha kuwa Tanzania inahitaji rais muadilifu, awe mtumishi mwema,na awe kimbilio la watu.
Amesema
mgombea wa CCM Dr John Magufuli hana sifa za uadilifu kwa kuwa wizara
ya ujenzi aliyoiongoza kwa miaka mingi, kitengo cha mizani kina kashfa
kubwa za rushwa.
Amesisitiza kuwa wizara hiyo inaongoza kwa rushwa.
Pia amemtuhumu Dr Magufuli kwa kununua meli ya miaka 30 kwa gharama ya meli mpya.
“Wizara ya ujenzi inaongoza kwa ufisadi,Je Magufuli ni mwadilifu?,” alihoji Sumaye.
“Ameshindwa kupambana na ufisadi wizarani kwake ataweza kwa nchi?”
“Lazima rais awe msikivu,je Magufuli ni msikivu?”
“Kigamboni aliwaambia watu wapige mbizi Maana yake wafe.”
Post a Comment